Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, hatua za ukandamizaji za ukoo wa Aal Khalifa tangu vita vya kulazimishwa vya Ramadhani hadi sasa dhidi ya Mashia wa Bahrain zimeongezeka kwa kiwango kikubwa. Kukamatwa na kuteswa wananchi wa Bahrain pamoja na kufukuzwa na kuvuliwa uraia makumi ya Wabahrain, ni miongoni mwa hatua za ukandamizaji zinazofanywa na utawala wa kidikteta wa Aal Khalifa. Vikosi vya usalama vya utawala wa Aal Khalifa, kwa kuvamia kwa ukatili nyumba za wanazuoni wa Kishia katika maeneo mbalimbali ya Bahrain, vimewakamata maulamaa na wanazuoni wa dini.
Wimbi hili kubwa la kukamatwa kiholela linalofanywa na utawala wa Aal Khalifa, linaonesha kuendelea kuongezeka kwa mkabala wa kiusalama na utekelezaji wa sera za ukandamizaji wa kimfumo dhidi ya wananchi wanaotekeleza haki yao ya kutoa kwa njia ya amani maoni na misimamo yao ya kisiasa inayohusiana na vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran pamoja na athari zake za moja kwa moja kwa Bahrain.
Kufuatia matukio haya, mamlaka za Bahrain zimewakamata zaidi ya wananchi 300 wakiwemo wanawake na watoto, na zimemuua mwananchi mmoja nje ya mfumo wa sheria.
Kwa ajili ya kupata ufafanuzi zaidi kuhusu jinai za utawala dhalimu wa Aal Khalifa, tulifanya mazungumzo na Baqir Darwish, rais wa Jumuiya ya Haki za Binadamu ya Bahrain, ambayo mnayasoma hapa chini:
Lengo la kukamatwa kwa kiwango kikubwa kwa wanazuoni na maulamaa nchini Bahrain na vikosi vya usalama vya utawala wa Aal Khalifa ni nini? Umoja wa Falme za Kiarabu una nafasi gani katika jinai hizi?
Maafisa wa usalama wa Bahrain, kwa kuchochewa na Umoja wa Falme za Kiarabu, wako katika juhudi za kuiangamiza jamii ya Mashia, kiasi kwamba hawakubali tena uhuru wa mambo ya dini kutoka serikalini, kutounga mkono kwa duru za wanazuoni na jamii ya Kiislamu ya Bahrain vita vya kivamizi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, pamoja na upinzani wa wanazuoni wa Bahrain dhidi ya miradi yote ya kuhalalisha uhusiano na utawala vamizi.
Ukandamizaji huu dhidi ya Mashia haujawahi kushuhudiwa katika historia ya kisiasa ya Bahrain; miongoni mwa waliokamatwa wapo wanazuoni wakubwa, maimamu wa Swala za Ijumaa na Jamaa, wakurugenzi wa Hawza za elimu, wawakilishi wa Mara'ji' wa dini huko Najaf Ashraf na Qum Tukufu, walimu wa Hawza, makhatibu na wabebaji wa ujumbe wa dini; pia baadhi ya wanachama waanzilishi wa “Baraza la Kiislamu la Wanazuoni” lililokuwa chini ya uongozi wa Ayatollah Sheikh Isa Qassim wanaonekana miongoni mwao.
Taarifa za Wizara ya Mambo ya Ndani zinazungumzia nafasi ya Hawza za elimu, vikundi vya Husseiniyya, misikiti, shule za watoto, taasisi za Kiislamu na hata hukumu za kifiqhi; jambo linaloonesha kwamba; serikali inajiandaa kutekeleza kampeni kubwa ya vikwazo dhidi ya vituo vyote hivi vinavyohusiana na Mashia.
Serikali hata imeenda mbali zaidi na kuanza kuhalalisha uhalifu dhidi ya itikadi za Mashia; kiasi kwamba inaelezea “Wilayat al-Faqih” kuwa ni ugaidi, ilhali ugaidi wa kweli upo katika kambi za kijeshi za Marekani nchini Bahrain.
Wanazuoni, wasomi na wanafikra wa ulimwengu wa Kiislamu wana jukumu gani mbele ya Mashia wanaodhulumiwa nchini Bahrain?
Ni muhimu kwa wanazuoni na wanafikra kutoa taarifa za kulaani uchochezi huu wa kimadhehebu dhidi ya Mashia wa Bahrain na kusisitiza umuhimu wa kuheshimu wingi wa dini na haki za wananchi; pia kuelezea yanayotokea kuwa ni jinai dhidi ya itikadi na imani za Mashia duniani kote.
Kutolewa kwa misimamo na taarifa za kulaani kutoka kwa maimamu wa Ijumaa, Hawza za elimu na taasisi za Kiislamu dhidi ya ukandamizaji wa kimadhehebu dhidi ya Mashia nchini Bahrain kutakuwa na athari kubwa na muhimu.
Vyombo vya habari vina jukumu na risala gani katika kufafanua jinai zinazokiuka haki za binadamu nchini Bahrain?
Vyombo vya habari vina jukumu la kimaadili na kitaaluma la kufichua ukweli na kuakisi mateso na matatizo ya wananchi, ikiwa ni pamoja na kupitia kuonesha wazi ukiukwaji wa haki na uhalifu. Aidha, uandishi wa habari unazuia suala hili kutengwa na fikra za umma wa kimataifa na husaidia kuunda shinikizo la kweli la kupambana na kuenea pamoja na kuongezeka kwa mateso na ubaguzi wa kimadhehebu dhidi ya Mashia wa Bahrain.
Kwa msingi huo, kuna haja kubwa ya vipindi vya televisheni na redio, ripoti za habari pamoja na kampeni za vyombo vya habari vya mshikamano katika mitandao ya kijamii.
Maoni yako